Naibu Waziri apiga marufuku eneo la Shule kutumika kibiashara |
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo, ameuagiza uongozi wa
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, kufuta mawazo ya kubadilisha matumizi
Shule ya Msingi Uhuru Wasichana kama eneo la kibiashara.
Aidha amemtaka Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Isaya Mngurumi, kutoa
kipaumbele kwenye malipo ya fedha za likizo na kupandishwa daraja kwa
walimu wa shule hiyo, kutokana na kufanya kazi kwenye mazingira magumu.
Pia amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa kuhakikisha kuwa Shule hiyo
haikosi karatasi maalum za kuchapishia maandishi ya nukta nundu, kwa
wanafunzi wasioona.
Naibu Waziri alitoa maagizo hayo Dar es Salaam, tarehe 17 februari 2016
wakati alipotembelea shule hiyo ili kufahamu changamoto mbalimbali
zilizopo.
Alisema lazima maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ya
kutaka Shule ya Uhuru wasichana isibadirishwe na kutumika kwa matumizi
ya kibiashara yatekelezwe.
Mheshimiwa Jafo aliitaka halmashauri hiyo kuboresha miundombinu ya shule
ili iendelee kutoa elimu kwa watoto kwa sababu bado serikali inahitaji
uwepo wa shule za kutosha.
“Kama bado mna mawazo ya kubadirisha matumizi ya shule ya Uhuru
wasichana ni bora muyafute, nataka maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu,
yatekelezwe†alisisitiza.
Mheshimiwa Jafo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, alionyesha
kusikitishwa na mazingira magumu wanayokabiliana nayo walimu wa shule ya
Uhuru mchanganyiko, ambao wanafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri alimuagiza Mkurugenzi na Ofisa Elimu
wa halmashauri hiyo, kuongeza magodoro yanayotumiwa na wanafunzi hao
kufanyia mazoezi.
Aliongeza kuwa, walimu wa shule hiyo wanapaswa kupewa kipaumbele kwenye
malipo ya likizo pamoja na kupandishwa madaraja kutokana na kufanyakazi
kwa moyo wa kujituma.
“Mkurugenzi sitaki kusikia malalamiko kuhusu kucheleweshwa malipo ya likizo au kupandishwa madaraja kwa walimu hawa.
“Wamekuwa wakifanya kazi kwenye mazingira magumu lakini kwa moyo wa
kujitolea hivyo nataka wawe wanapewa kipaumbele zaidi kwenye maslahi
yao†alisema.
Naibu Waziri alisema, serikali itatilia mkazo upatikanaji wa vifaa
maalum vya kufundishia ili wanafunzi wenye mahitaji maalum waweze kusoma
bila vikwazo vyovyote.
Aliwataka wazazi walio na watoto wenye ulemavu, kutowaficha majumbani bali wawapeleke shuleni kupata taaluma.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Anna Mshana, alimpongeza
Waziri Jafo kwa kufika kujionea changamoto zilizopo ili ziweze kufanyiwa
kazi.
Alisema, wanafunzi wenye mahitaji maalum wanahitaji uwepo wa vifaa vya kutosha vya kujifunzia.
Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1921, ina wanafunzi 64 wasioona, 22
viziwi pamoja na upofu, 79 wenye mtindio wa ubongo pamoja na wanafunzi
watano wenye ulemavu wa ngozi.
0 comments:
Post a Comment